Wakala wa Nishati vijijini (REA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Umeme Tanzania (TANESCO) imefanya uzinduzi wa Mradi kabambe wa Umeme vijijini kwa Mkoa wa Arusha katika kijiji cha Digodigo, kata ya Digodigo, Tarafa ya Sale Wilaya ya Ngorongoro. Uzinduzi huu ulifanywa na Naibu Waziri wa Nishani na Madini Mheshimiwa Medard Kalemani ikiwa Lengo ni kufikisha Nchi katika uchumi wa kati pamoja na kurahisisha upatikanaji na utoaji huduma kwa Wananchi.
Uzinduzi huu ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Vyama na Serikali akiwepo Mhe. Wiliam Tate Olenasha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hili la Ngorongoro, Bwana Richard Kwitega Katibu Tawala Mkoa akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Rashid Mfaume Taka Mkuu wa Wilaya Ngorongoro, Mheshimiwa Mathew Eliakimu Siloma Mwenyekiti wa Halmashauri, Bwana Raphael John Siumbu Mkurugenzi Mtendaji Wilaya, pamoja na viongozi wengine wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Mhe. Mgeni rasmi katika salamu zake aliwashukuru wananchi wa kata ya Digodigo kwa kujitokeza kwa wingi na kwa dhati na kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa mapokezi ambayo ameyapata. Aidha Mheshimiwa Naibu Waziri alimpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuwatumikia wananchi wote na aliahidi kufikisha salamu za wananchi wa Ngorongoro kwa Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Waziri alisema anazindua mradi huu katika Wilaya ya Ngorongoro kata ya Digodigo kwa wananchi wote wa Mkoa wa Arusha, wenye wilaya sita (6), majimbo saba (7) ambapo jumla ya vijiji 242 katika Mkoa wa Arusha vitasambaziwa umeme huo.
Mheshimiwa Naibu Waziri alisema atawatambulisha wakandarasi wawili ambao watabaki kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye vitongoji vyote, kaya zote, nyumba kwa nyumba. Umeme huo utaenda katika Taasisi zote za Umma, Shule, Makanisa, Misikiti, Mitambo yote ya maji katika Mkoa wa Arusha na kusema kuwa Mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini kila Mtanzania atatumia umeme huo.
Mheshimiwa Naibu Waziri alisema kuwa zote ni juhudi za Mheshimiwa Mbunge ambaye alikuwa akimkumbusha mara kwa mara katika kuwaletea Maendeleo Wananchi wa Wilaya Ngorongoro, alisema mradi huu kwa Ngorongoro utafungwa kwa vijiji thelathini na tatu (33) na vitongoji vyake, aidha ifikapo Machi 2019 vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Waziri aliwakaribisha na Kuwatambulisha wakandarasi wawili ambao mmoja atafanya kazi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji na mwingine kupeleka umeme kwenye vijiji.
Wakandarasi hao ni Nipo Group ambaye atafanya kazi ya Kupeleka umeme kijiji kwa kijiji, Kitongoji kwa kitongoji na nyumba kwa nyumba bila kujali aina ya nyumba.
Mkandarasi wa Pili ni Angelique Int. Ltd kutoka India ambaye atapeleka umeme katika vitongoji hamsini na saba (57) na kusambaza nyumba kwa nyumba. Kazi hii itafanywa kwa muda wa miezi ishirini na nne (24) ambapo miezi 18 kukamilisha mradi na miezi 6 kurekebisha maeneo madogo madogo.
Mheshimiwa Naibu Waziri alisema kuwa hatotarajia kijiji kurukwa na endapo wataweka wakandarasi wasaidizi basi watumie wananchi wa eneo husika ili kusudi wapate ajira na kusisitiza kuwa walipwe ujira wao papo kwa hapo na kuwasisitiza wananchi kufanya kazi usiku na mchana na kusema kuwa Mradi huu utagharimu kiasi cha Takriban Bilioni 40, alisisitiza TANESCO na REA kuwasimamia wakandarasi hao ili kupata thamani ya fedha.
Majukumu makuu waliopewa TANESCO ni pamoja na kuwafuata wateja na kuhakikisha watafungua kituo kidogo cha umeme ili wateja waweze kuja kulipia Tsh. 27,000/= katika ofisi hizo ikiwa ni gharama ya kufungiwa umeme. Aliwaagiza TANESCO kupanga nyumba katika maeneo yenye watu wengi na kuanzisha dawati la huduma katika kata ya Digodigo ndani ya siku saba. Mheshimiwa Naibu Waziri aliwatahadharisha wananchi kuepuka matapeli na walanguzi na kusisitiza kuwa bei ya kufunga umeme ni Tsh. 27,000 tu na siyo vinginevyo. Ili kuepuka walanguzi mheshimiwa Naibu Waziri aliwataka TANESCO kuwaidhinisha wakandarasi wote na kuhakikisha kuwa TANESCO inaratibu bei zao. Mheshimiwa Naibu Waziri alitoa taadhari kuwa endapo vishoka watajitokeza Mkuu wa Wilaya atachukua hatua stahiki.
Mheshimiwa Naibu Waziri alisema kuwa kwa wateja wa awali 200 watapewa kifaa cha kufunga umeme bure na endapo wananchi watachelewa watapata kifaa hicho kwa gharama ya Tsh. 36,000. na aliwapatia Wazee sana mita za umeme kumi (10) bure. Chombo hicho alisema kitaweza kuunganisha jiko la umeme, Jokofu, pamoja na Kuchaji simu. Aliomba na kusisitiza wananchi wote kutumia umeme huo kukuza uchumi kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo kama vile vya kukoboa mahindi.
Mheshimiwa naibu Waziri aliweka jiwe la msingi kuashiria kuzindua umeme rasmi kwa Mkoa mzima wa Arusha mnamo tarehe 19.08.2017 katika eneo hilo.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.