Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mheshimiwa Rashid Mfaume Taka Mgeni Rasmi akiongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ngorongoro Ndugu Raphael John Siumbu pamoja na baadhi ya wataalamu kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro wamezindua ujenzi wa Chuo kikubwa cha Ufundi Stadi (VTC) mnamo Tarehe 18/08/2017 ambapo Chuo hicho kinajengwa kwa Nguvu za Wananchi wa Kata ya Samunge.
Akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa chuo hicho Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi Ndugu Sakanda Gaima amesema ujenzi huo unatarajia kuanza mwezi Agosti 2017 na kukamilika mwezi Agosti 2018, Aidha amemwambia Mgeni Rasmi kuwa Chuo hicho kitakuwa mali ya Serikali hivyo baada ya majengo kukamilika Chuo kitakabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya kwa uendeshaji. Vile vile Mwenyekiti amemwambia Mgeni Rasmi kuwa kwa sasa mradi huu unahitaji kuwa na mtaalamu mwelekezi ili uweze kutekelezwa kwa ubora unaotakiwa kitaifa na Mamlaka ya Ufundi Stadi(VETA).
Mgeni Rasmi Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya akipokea taarifa hiyo amepongeza jitihada hizo na kuwashukuru wananchi wa Samunge kwa uamuzi huo ambapo amesema atahakikisha anausimamia mradi huu na kwamba ameagiza Halmashauri ya Wilaya kutoa watalaamu wa ujenzi ili kufanya mambo yote yanayotakiwa katika hatua za awali kwa muda usiozidi wiki moja. Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya pia amesema kwa sasa macho ya Halmashauri na Wilaya kwa ujumla yatakuwa kwenye mradi huo mpaka utakapokamilika. Mwisho Mheshiwa Mkuu wa Wilaya aliuomba uongozi wa Serikali ya kijiji cha Samunge kutenga eneo zaidi ili kufanikisha ujenzi wa chuo hicho.
Nae Mkurugenzi Mtendaji Bwana Raphael John Siumbu amesema Halmashauri ipo tayari kushiriki moja kwa moja katika ujenzi wa Chuo hicho na kwamba Halmashauri itatoa wataalamu wa Ujenzi ili kusimamia mradi huo na itatenga fedha za mapato ya ndani kadri itakavyowezekana kushiriki kuwezesha ujenzi huo.
Wakitoa Salamu viongozi wa kijamii waliohudhuria kwenye hafla hiyo ya uzinduzi wa ujenzi wa Chuo hicho wamesema wananchi wa Samunge wanajenga Chuo cha Ufundi Stadi ili kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Daktari John Pombe MAGUFULI za kuanzisha Tanzania ya Viwanda, wamesema Rais ameonesha nia ya kuanzisha Viwanda hapa Nchini na wao wanajenga Chuo cha Ufundi ili kuzalisha wataalamu watakaofanya kazi viwandani. Viongozi hao pia wamesema mradi huu utatekelezwa kwa kushirikiana na Serikali na hawatakubali mradi huu utumike kisiasa kabisa.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.