Wasichana wa Shule za Msingi na Sekondari leo tarehe 25/04/2018 wamejitokeza kwa wingi kupata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi katika Wilaya ya Ngorongoro Mkoani Arusha.Tukio hilo lilitokea wakati Mkuu wa wilaya ndugu Rashid Mfaume Taka alipofanya Uzinduzi wa chanjo hiyo katika zahanati ya Soitsambu iliyoko katika kata ya Soitsambu. Katika uzinduzi huo mratibu wa zoezi hilo Dr Emmanuel Mallange (Kaimu mganga mkuu wa wilaya) akishirikiana na timu ya madaktari na wauguzi walitoa elimu juu ya saratani ya mlango wa kizazi.
Chanjo hiyo ya saratani ya mlango wa kizazi itatolewa kwa watoto wote wa kike waliopo mashuleni na majumbani wenye umri wa miaka kuanzia miaka 14 na itaendelea kutolewa kwa muda wa wiki nzima katika wilaya ya Ngorongoro. Mratibu wa chanjo hiyo Dr Emmanuel Mallange alifafanua kuwa Tanzania inaungana na dunia katika kuadhimisha wiki ya chanjo duniani tarehe 25 hadi 30 mwezi Aprili 2018. Katika wilaya ya Ngorongoro jumla ya wasichana 3645 wa shule za msingi na sekondari wamesajiliwa kwa ajili ya kupata chanjo hiyo na vituo vyote vya kutolea huduma wilayani vitakuwa wazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni.
Katika wiki hii ya chanjo wasichana wanaopata chanjo watapatiwa shuleni kwa walioko shuleni na walioko majumbani itatolewa katika vituo vya afya au vituo vya kutolea huduma. Chanjo hii ni bure hivyo walengwa wote wajitokeze.
Chanjo itatolewa kwa wasichana waliofikisha umri wa miaka 14 na ili kupata kinga kamili walengwa watahitaji kupatiwa dozi ya pili baada ya miezi 6. Chanjo hii haina madhara na ni muhimu kwa ajili ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi.
Saratani hii husababishwa na virusi vinavyojulikana kitaalamu kama human papilloma virus(HPV) na dalili zake ni maumivu ya mgongo, miguu ,kiuno, kuchoka, kutokwa damu baada ya kujamiiana, kuvimba mguu upande mmoja na kutokwa uchafu wa kahawia kwenye uke. Dalili mbaya zaidi ni figo na ini kushindwa kufanya kazi pamoja na kupatwa na fistula.
Nchini Tanzania saratani ya mlango wa kizazi ni ya kwanza kwa vifo ikifuatiwa na saratani ya matiti "Saratani hizi mbili kwa pamoja husababisha zaidi ya asilimia 50 ya vifo vyote vya wakinamama vitokanavyo na saratani" alibainisha Dr Mallange.
Katika uzinduzi huo Mkuu wa wilaya aliambatana na wageni wengine akiwemo Kaimu Katibu Tawala ndugu William Ndossi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wilaya Ngorongoro ndugu Emmanuel Sukums, wakuu wa idara kutoka Halmashuri , mwenyekiti wa halmashauri Mhe. Mathew Siloma, makamu mwenyekiti Mhe. Emmanuel Shangai na madiwani wengine.
Akizungumza katika uzinduzi huo mwenyekiti wa huduma za kijamii mheshimiwa Johanes Tiamasi (Diwani wa kata ya Kakesio) aliwasihi viongozi wote katika ngazi za vijiji na kata wahakikishe kuwa wanatoa hamasa kwa walengwa ili zoezi hili liwafikie walengwa wote katika wilaya ya Ngorongoro.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.