Ofisi ya Rais - Tamisemi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa amekabidhi magari 10 kwa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) huku magari tisa (9) yakipelekwa katika ofisi za TSC ngazi ya Wilaya.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi magari hayo iliyofanyika tarehe 11 Agosti, 2024 katika Ofisi za TAMISEMI Mtumba jijini Dodoma, Waziri Mchengerwa alisema kuwa Serikali inatambua kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa magari katika Ofisi za TSC 139 zilizopo katika kila wilaya nchini.
Alisema kuwa magari 10 yaliyotolewa ni mwanzo wa kuanza kuboresha mazingira ya utendaji kwa Makatibu Wasaidizi ili waweze kutekeleza mjukumu yao kwa ufanisi.
“Ikumbukwe kuwa Serikali imekwisha toa magari kwa Makatibu Tawala Wasaidizi Seksheni ya Elimu wote nchini, Wakuu wa Divisheni za Elimu Msingi na Sekondari wote na sasa tumeanza kwa Makatibu Wasaidizi wa TSC wa Wilaya,” alisema.
Alisema lengo la kutoa magari hayo ni kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za elimu zinazofanyika katika ngazi ya shule pamoja na kuwafikia walimu katika vituo vyao ili kuwasilikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.
Mhe. Mchengerwa alisema kuwa jukumu la usimamizi wa Elimu linahitaji uwajibikaji na usimamizi thabiti katika ngazi ya Taifa, Mikoa, Halmashauri, Kata na Shule.
Alisema kuwa pamoja na bidii, weledi, ubunifu, uaminifu na utiifu, mafanikio katika usimamizi wa elimu yanategemea pia uwezeshwaji wa vifaa na vitendea kazi ikiwemo vyombo vya usafiri.
Mhe. Mchengerwa aliongeza kuwa matarajio ya Serikali ni kuwa, magari waliyokabidhiwa yatakuwa nyenzo muhimu kwa viongozi wakiwemo Makatibu Wasaidizi wa Wilaya katika usimamizi na ufuatiliaji wa Elimu nchini ikiwa ni pamoja na utatuzi wa kero zinazojitokeza.
Aidha , Waziri alielekeza kuwa magari hayo yatunzwe vizuri ili kuweza kuongeza ufanisi na ubora wa elimu katika utekelezaji wa majukumu ya kuwahudumia walimu ili wapite salama katika mzunguko wao wa ajira.
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.