ZOEZI LA KUOGESHA MIFUGO LAFANYIKA KATIKA KIJIJI CHA OLOIPIRI
Ngorongoro , ARUSHA
Zoezi la kuogesha mifugo kitaifa limeanza rasmi leo na Wilayani Ngorongoro katika kata ya Oloipiri.Akizungumzia zoezi hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Rafael Siumbu amesema kuwa zaidi ya asilimia 70% ya magonjwa yanayoua mifugo ni magonjwa ya nayosababishwa na wadudu kama kupe ,mbungo na chawa hivyo zoezi hili litasaidia sana kupunguza vifo vya mifugo.Bwana Raphael Siumbu ameendelea kuwasihi wafugaji wazingatie maelekezo ya madaktari na kuogesha mifugo yao mara kwa mara ili kupunguza vifo vya mifugo visivyo vya lazima vinavyompelekea mfugaji kupata hasara.
Akizungumza na wananchi Ndugu Ally Karanjai ambaye ni Mwenyekiti wa wazazi Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ngorongoro amefurahishwa na zoezi hilo na kuwasihi wanachi wawe wazalendo na serikali inatekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi na kuwasihi ni jukumu lao kusimamia na kuhakikisha mifugo wanaogeshwa ili kuepukana na magojwa yanayoletwa na kupe.
Akizungumzia zoezi hilo Bwana Chobi Chubwa Afisa Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Ngorongororo Serikali imetoa Chupa 6 za ujazo wa lita moja na Robo lita na kufanya jumla ya lita 6 na robo za dawa kwaajili ya kila josho wa majosho 23 yanayofanya kazi na itatumika kwa muda wa miezi .Amesisistiza kuwa ngombe 2,000 wa kwanza kufika kwa kila josho wataogeshwa bure na baada ya hapo kichwa cha ngombe kitalipiwa sh.100 na mbuzi sh 50 na fedha hizo zitakusanya na kamati maalumu ya watu watano wanaosimamia josho.Ameongeza kusema kuwa fedha hizo zinazokusanywa, ofisi ya Mkurugenzi mtendaji itawasaidia kamati hizo za usimamizi kuwaunganisha na msambazaji wa dawa za mifugo aliyeteuliwa na Serikali ili waweze kupata dawa ili zoezi ilo liwe endelevu. Pia ameongeza kuwa hadi kufikia jana wamefanikiwa kuogesha ngombe 3800 huku wakitegemea idadi kuongezeka zaidi kwa siku ya kesho.
Kwa upande wa wananchi Bw Elikana Sayori mkazi wa kijiji cha Kirtalo amesema changamoto wanayokumbana nayo zaidi ni magojwa yaenezwayo na kupe lakini pia suala la malisho ya mifugo kutokuwa na mipaka,na kupelekea mwingiliano wa mifugo baina ya vijiji.Sambamba na hivyo wananchi hao wameiomba serikali kuanzisha zoezi la upimaji wa vijiji ili kubainisha mipaka na kurahisisha utaratibu wa ufugaji wenye tija na kuondoa migogoro.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro
Bwana Chobi Chubwa Afisa Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Ngorongoro akitoa maelekezo yaliyotolewa na serikali baada ya kutembelea Josho la kijiji cha Soitsambu
Viongozi wa Chama cha mapinduzi wilaya ya ngorongoro Amosi Shimba (Katibu wa CCM wilaya ya Ngorongoro) na Bw. Ally Karanjai (Mwenyekiti wa wazazi wilaya ya Ngorongoro) walipotembelea josho la kijiji cha Oloipiri kujionea shughuli ya uogeshwaji wa mifugo ikiendelea na kukabidhi dawa zilizotolewa bure na serikali awamu ya tano kwaajili ya kuendesha zoezi hilo
Hakimiliki©2017 NDC . Haki zote zimehifadhiwa.